Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Kimura Mitsuhiro, Rais wa Chama cha Wazalendo wa Japan (Issuikai), katika ujumbe alioutuma kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Kituo cha Tafiti za Mpango wa Ustaarabu wa Dunia uliofanyika Ankara, alikosoa sera za Marekani na mfumo wa sasa wa dunia, akazungumzia kuibuka kwa mfumo wa dunia wa ncha nyingi na kusisitiza umuhimu wa mataifa ya Asia kuwa huru na kujitegemea.
Utawala wa dunia wa ncha moja unaoongozwa na Marekani unaporomoka
Mitsuhiro alisema kuwa; dunia inapitia kipindi cha kihistoria chenye mabadiliko makubwa, na kwamba mfumo wa utawala wa ncha moja unaoongozwa na Marekani unaendelea kuporomoka huku mfumo mpya wa dunia wa ncha nyingi ukiendelea kujengeka.
Akikosoa sera za Marekani za kuingilia masuala ya mataifa mbalimbali duniani alisema: "Mashambulizi yasiyo ya haki ya Marekani dhidi ya Iran, kama ilivyo kwa uingiliaji wake wa kijeshi katika nchi za Amerika ya Kusini, ikiwemo Venezuela, hayawezi kukubalika kwa namna yoyote ile."
Rais huyo wa Chama cha Wazalendo wa Japan pia alizungumzia mgogoro unaoikabili kambi ya Magharibi na Shirika la Mkataba wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO). Akikumbusha kauli ya Emmanuel Macron aliyeliita NATO shirika lililokumbwa na "kifo cha ubongo", na kulinganisha kwa Donald Trump muungano huo na "chui wa karatasi", alisema hali hiyo ni matokeo ya mwelekeo unaoongezeka wa mataifa huru kutaka kulinda mamlaka yao ya kitaifa na kujiamulia hatima yao wenyewe.
Iran, Urusi, Uturuki na China ni mhimili wa amani barani Asia
Mitsuhiro akizungumzia kudhoofika kwa mfumo wa Atlantiki na kuimarika kwa mhimili wa Eurasia alisema: "Mataifa muhimu kama Iran, Uturuki, Urusi na China yanajitahidi kuhifadhi amani, utulivu na kuhakikisha maisha na ustawi wa wananchi."
Aliongeza kuwa; mbele ya uchochezi wa mfumo wa ubepari wa kimataifa, watu huru na wenye uelewa duniani kote wanaendelea kusimama imara na kupinga.
Kambi za kijeshi za Marekani zinapaswa kuondolewa Japan
Rais wa Chama cha Wazalendo wa Japan, alikosoa utegemezi wa nchi yake kwa Marekani tangu baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia na akataka kukomeshwa kwa uwepo wa kijeshi wa Washington nchini Japan.
Alisema: "Baada ya Japan kushindwa katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, nchi yetu iliingia katika mfumo wa utegemezi kwa Marekani. Tunataka kambi za kijeshi za Marekani ziondolewe nchini Japan, na tunaunga mkono kuanzishwa kwa mfumo maalumu wa usalama wa Asia unaojengwa juu ya msingi wa amani na utulivu kwa kushirikiana na nchi jirani."
Wakati wa kufufua hekima ya Mashariki umefika
Mitsuhiro alieleza matumaini yake kuwa; Mkutano wa Kituo cha Tafiti za Mpango wa Ustaarabu wa Dunia, uliofanyika tarehe 18 na 19 Julai mjini Ankara, utasaidia kuimarisha mikondo inayopinga NATO na kuweka msingi wa kuibuka kwa ustaarabu mpya wa Mashariki. Aidha, alisisitiza nafasi ya kihistoria ya Uturuki na Japan katika ustaarabu wa mwanadamu.
Mwishoni mwa hotuba yake, akirejelea nadharia ya "Kuporomoka kwa Magharibi" ya mwanafalsafa wa Kijerumani Oswald Spengler, alisema: "Mfumo wa kibepari wa kinyonyaji, ambao umesababisha kudhoofika kwa roho ya mwanadamu na kusambaratika kwa miundo ya kijamii, umeendelea kuishi kwa kutegemea nguvu za kijeshi na mabavu pekee. Hata hivyo, sasa umefika wakati wa mfumo huo kuporomoka. Leo ni wakati wa hekima halisi ya Mashariki pamoja na utamaduni wa mshikamano na maelewano ya Asia kuwa kitovu cha mjadala na kupewa nafasi inayostahili."
Maoni yako